Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli jana tarehe 28 Juni, 2020 amekagua maendeleo ya ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (standard gauge) kwa sehemu ya kwanza ya Dar es Salaam – Morogoro na kuelezea kuridhishwa kwake na maendeleo ya ujenzi wa mradi huo mkubwa.
Rais Magufuli alisafiri kwa gari kandokando ya reli hiyo kuanzia Kisarawe hado Soga Mkoani Pwani na kisha akapanda kiberenge kilichopita katika reli hiyo mpya kuanzia Soga hadi Kikongo kabla ya kuendelea na safari yake kwa gari kuelekea Morogoro.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) Mhandisi Masanja Kadogosa alimueleza Rais Magufuli kuwa kazi ya ujenzi wa sehemu ya kwanza ya reli hiyo imefikia asilimia 82 ambapo Watanzania 13,000 wamenufaika na ajira na inatarajiwa kukamilika mwisho wa mwaka huu (2020).
Akizungumza na wananchi wa Soga na Kikongo, Rais Magufuli amewapongeza kwa kupata mradi huo na ametaka waendelee kuchapa kazi kwa juhudi na maarifa ili waweze kunufaika zaidi na mradi huo.
Aidha, Rais Magufuli alisikiliza kero za wananchi hao ambapo aliendesha harambee ya kuchangisha fedha kwa ajili ya uboreshaji wa Shule ya Msingi Soga na kufanikiwa kukusanya shilingi 68,535,000/- zikiwemo shilingi Milioni 5 alizochangia yeye mwenyewe, na amemtaka Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi kufika Kijijini hapo ili kutatua mgogoro wa ardhi kati ya wananchi na mmiliki wa shamba kubwa lililopo kijijini hapo ambalo halilimwi.
Rais Magufuli pia amemuagiza Waziri wa Maji Prof. Makame Mbarawa kuhakikisha anatatua tatizo la maji linalokikabili kijiji cha Soga.
Ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imechukua hatua madhubuti za kutekeleza mradi huo ambao utagharimu shilingi Trilioni 7.02 kwa sehemu ya kuanzia Dar es Salaam hadi Makutupora Mkoani Dodoma, pamoja na kutekeleza mradi mkubwa wa uzalishaji wa megawati 2,115 za umeme katika Bwawa la Nyerere ili kukuza uchumi wa Watanzania na kuinua kipato cha wananchi na hivyo amewataka Watanzania wote kuunga mkono juhudi hizo.
Akiwa Mlandizi, Rais Magufuli amesikiliza kero za wananchi na kumuagiza Naibu Waziri wa Maji Juma Aweso kuhakikisha Wizara ya Maji inatatua tatizo la maji la Mitaa ya Mbwawa Shule na Mbwawa Mkoleni na pia amemuagiza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe kuanza mchakato wa ujenzi wa barabara ya lami ya Mafia – Mzenga – Vikumbulu ili kuunganisha Mlandizi na reli.
Rais Magufuli amewasili Mjini Morogoro na leo ataendelea na ziara yake Mkoani hapa ambapo ataweka jiwe la msingi la ujenzi wa mahandaki ya reli ya kisasa (standard gauge) sehemu ya Morogoro – Makutupora, kuzindua barabara ya lami ya Rudewa – Kilosa na atafanya mkutano wa hadhara katika eneo Mkadage Wilayani Kilosa.
Rais Magufuli amewataka Watanzania wote kujiandaa kwa Uchaguzi Mkuu utakaofanyika baadaye mwaka huu (2020) huku wakikumbuka kudumisha amani, umoja na mshikamano pamoja na kuwachagua viongozi watakaowafaa.
0 Comments