Na Jackline Kuwanda,DODOMA
Baada ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe kushambuliwa na kujeruhiwa na watu wasiojulikana wakati akirejea nyumbani kwake,kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Gilles Muroto amesema kuwa jeshi la polisi Mkoani humo linafanya uchunguzi wa kina ili kupata ukweli na usahihi wa tukio hilo.
Kamanda Muroto ametoa kauli hiyo leo Mkoani humo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na tukio hilo
Wakati huo huo kamanda Muroto amepiga marufu kwa wale watakao ingilia uchunguzi wa jeshi la polisi huku akiwataka watu kutotumia tuko hilo kama mtaji wa kisiasa.
Amesema jeshi hilo lilipokea taarifa za kushambuliwa kwa mwenyekiti wakati alipokuwa akirejea nyumbani kwani baada ya kufika nyumbani na kushushwa na Dereva pindi alipokuwa akipandisha ngazi kwenye nyumba yake inadaiwa kuwa alikutana na watu watatu walikuwa wamevalia jaketi ambapo walianza kumshambulia kwa kumkanyaga na mateke na hasa kwenye mguu wake wa kulia.
Hata hivyo amesema kuwa tukio hilo litachunguzwa kama matukio mengine na kadiri watakavyokuwa wakisonga mbele taarifa zitatolewa.
Ikumbukwe kuwa tukio la kushambuliwa na watu wasiojulikana kwa viongozi wa ngazi za Juu wa CHADEMA litakuwa la pili kutokea hapa jijini Dodoma baada ya miaka mitatu kupita tangu mwaka 2017 ambapo Mwanasheria wa Chama hicho,Tundu Lissu alipofyatuliwa risasi na watu wasiojulikana huku jeshi la Polisi likiendelea na mkakati kabambe wa kufanya uchunguzi wa Matukio hayo .
0 Comments