
Na Mathias Canal, NFRA-Morogoro
Mkutano
wa Baraza la wafanyakazi wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula
(NFRA) umejadili kwa kina ufanisi wa kazi pamoja na msisitizo kuhusu
maslahi ya wafanyakazi.
Katika
Mkutano wa Baraza hilo unaofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Ujenzi
mkoani Morogoro kwa siku mbili wafanyakazi wametoa maoni yao kuhusu
umuhimu wa kushirikishwa katika shughuli mbalimbali mara kwa mara ili
kutambua majukumu yanayofanywa na Taasisi hiyo.
Kadhalika
wafanyakazi wa Wakala wameomba kuendelea kujengewa misingi ya
uwajibikaji hasa katika kutambua wajibu wao kwa Umma na kusisitiza kuwa
watattekeleza majukumu yao pasina uzembe katika utekelezaji wa majukumu
yao.
Akizindua
Baraza hilo jana tarehe 21 Mei 2020 Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali
watu wa Wizara ya Kilimo Bi Hilda Kinanga wakati akimuwakilisha Katibu
Mkuu wa Wizara ya Kilimo Ndg Gerald Kusaya alisema si vema watumishi
kutumia muda mwingi katika kufanya shughuli ambazo hazina tija
zinazoathiri utendaji kazi.
Aliongeza
kuwa Serikali ya awamu ya tano inayo dhamira ya dhati ya kuondoa uzembe
na ubadhirifu miongoni mwa watumishi wa umma na hivyo mtumishi
anaruhusiwa kudai haki zile za msingi kwa kuzingatia Kanuni, Sheria na
Taratibu za Utumishi wa umma wakati wa kutekeleza wajibu wake wa msingi
kwa Mwajiri na kwa kutumia lugha ya staha.
Katika
siku mbili za Kikao cha Baraza wajumbe wamejadili masuala mbalimbali
yanayohusu Wakala na miongoni mwa ajenda hizo ni Kupitia Mpango wa
Biashara wa mwaka 2020/2021 (Business Plan), taarifa ya utekelezaji ya
robo ya tatu ya mwaka 2019/2020 na kupitia Rasimu ya Miundo mipya ya
Maendeleo ya Utumishi.
Wajumbe
wamejadili kwa kina agenda hizo muhimu kwa kuwa agenda ya kwanza
imewapitisha katika malengo/mipango ya Wakala, ya pili ni utekelezaji wa
majukumu ya Wakala uliofanyika kwa mwaka tulionao na tatu ni mpango wa
kuboresha maslahi ya wafanyakazi kwa lengo ya kuandaa majukumu mapya
yanayoendana na Muundo mpya wa Taasisi.
Pamoja
na kwamba wafanyakazi wa NFRA wamesisitiza umuhimu wa maslahi yao
lakini kwa nyakati tofauti katika michango yao wamesisitiza kuwa hakuna
haki bila wajibu hivyo wao wana wajibu muhimu wa kutekeleza majukumu yao
na ari kubwa.
“Kwa
kutambua uzito na umuhimu wa majukumu hayo kila mmoja wetu katika
sehemu yake ya kazi anatakiwa kuwajibika na kufanya kazi kwa bidii na
kwa uadilifu ili kuiwezesha Serikali kufikia malengo yake ya kukuza
uchumi na kuondoa umaskini kwa wananchi kwa kuwezesha nchi yetu kufikia
uchumi wa kati” Amekaririwa Meneja NFRA Kanda ya Sumbawanga Ndg Abdillah
Nyangasa
Afisa
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Ndg
Milton Lupa amesema kuwa bado Taasisi ina changamoto mbalimbali katika
utekelezaji wa majukumu ya kutoa huduma kwa umma ikiwemo ukosefu wa
rasilimali fedha na rasilimali watu wa kutosha, hali inayosababisha
kutofikiwa kwa malengo.
Lakini
amewahakikishia kuwa Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za
kutatua changamoto hizo ikiwemo kuiomba itupatie watumishi ili kukidhi
matakwa yetu.
Lupa
amesisitiza kuwa Watumishi wote wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa
kuzingatia Sheria, Kanuni na Maadili katika Utumishi wa Umma. Aidha,
Serikali haitasita kuchukua hatua kwa Mtumishi yoyote atakayejihusisha
na vitendo vya rushwa pamoja na vitendo vinavyokiuka maadili ya Utumishi
wa Umma.
0 Comments