Na Ismail Ngayonga-MAELEZO
SEKTA
ya Kilimo nchini imeendelea kuwa ni Sekta muhimu katika maendeleo ya
uchumi wa wananchi na Taifa kwa ujumla hususan katika wakati huu
tunapojizatiti kufikia uchumi wa viwanda.
Katika
kipindi cha miaka mitano, Pato la Taifa linalotokana na kilimo, kwa
kutumia bei za Mwaka 2015 limeongezeka kwa asilimia 17 kutoka Tsh.
Trilioni 25.2 Mwaka 2015 hadi Tsh. Trilioni 29.5 Mwaka 2019.
Vilevile,
sekta imeendelea kutoa ajira kwa Watanzania kwa asilimia 58 Mwaka 2018
na kuchangia asilimia 28.2 ya Pato la Taifa huku sekta ndogo ya mazao
ikichangia asilimia 16.2 na hiyo imetokana na kuongezeka kwa uzalishaji
wa bidhaa mbalimbali zikiwemo vyakula vinavyotokana na mazao ya kilimo.
Ili
kufikia kiwango malengo makubwa ya uzalishaji wa mazao, Sera
zinazoongoza utafiti zina mchango mkubwa katika kupanga maendeleo ya
sekta ya kilimo ikiwa ni pamoja na ya kuboreshea viwango vya maisha ya
wananchi kwa kuchochea ukuaji na kuongeza tija katika sekta muhimu za
uzalishaji za uchumi wa taifa.
Historia
inaonyesha kuwa nchi zilizozingatia sera zenye mwelekeo wa utafiti
thabiti zimefanikiwa kujenga uchumi wenye ushindani kwa kutumia
rasilimali walizonazo, na kuziendeleza kwa ajili ya kuboresha maisha ya
wananchi wao.
Katika
jitihada hizo, Serikali kupitia Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA)
imeendelea kuboresha uzalishaji wa mazao ya kilimo, mifugo, misitu na
uvuvi katika eneo la Tafiti na Ushauri elekezi ili kutoa huduma ya elimu
ya ushauri wa kitaalamu kwa wakulima.
Akiwasilisha
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2020/2021, Waziri
wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako anasema Serikali
kupitia SUA imeendelea na miradi mipya 13 ya utafiti yenye lengo la
kuboresha uzalishaji wa mazao ya kilimo, mifugo, misitu na uvuvi ili
kuwezesha wananchi kuzalisha mali na malighafi za mazao ya kilimo kwa
ajili ya viwanda.
Prof.
Ndalichako anasema Chuo hicho pia kimeweza huduma ya elimu ya ushauri
wa kitaalamu kwa wakulima 9,500 kwa kutumia vituo atamizi, mashamba
darasa, semina, kozi fupi, runinga na redio kwa lengo la kuongeza
uzalishaji wenye tija na kupunguza umaskini kwa wananchi.
‘Mafunzo
hayo yametolewa kwa wakulima katika mikoa ya Mwanza, Dar es Salaam,
Iringa, Dodoma, Tabora, Tanga, Pwani na Morogoro kwa lengo la kutoa
elimu kuhusu kilimo na ufugaji’’ anasema Prof. Ndalichako.
Aidha
Prof. Ndalichako anasema SUA pia ) imepima jumla ya sampuli 1,553
zikiwemo sampuli za udongo 1,180, za mimea 297, za mbolea za viwandani
20, za samadi tisa (9) na sampuli za maji 47 kutoka kwa watafiti
mashirika ya kilimo, Viwanda na Taasisi mbalimbali pamoja na wakulima
binafsi.
Waziri
Ndalichako anasema kuwa Serikali imeingia mikataba mipya 13 ya
mahusiano na Taasisi nyingine za ndani na nje ya nchi ili kuwajengea
uwezo wafanyakazi na wanafunzi katika kufanya tafiti za kisayansi na
kilimo kwa lengo la kuongeza uzalishaji wenye tija katika shughuli
mbalimbali za maendeleo kwa wananchi.
Anazitaja
taasisi hizo kuwa ni pamoja na Chuo Kikuu cha Sophia kilichopo Japan;
National Institute of Health - Korea; Foundation Pierre Fabre - France;
Kunming Institute of Zoology, Chinese Academy of Science; Silverlands
Tanzania Limited - Iringa, Tanzania; College of Animal Science and
Technology Nanjing Agricultural University - China; Agronomos Sin
Fronteras Foundation (ASFF ) - Iringa Tanzania; University of Leeds –
UK; na Wuhan University (WHU) – China.
Akifafanua
zaidi Prof. Ndalichako anasema katika kuboresha mazingira ya
kufundishia na kujifunzia Serikali imejenga jengo lenye uwezo wa
kuchukua wanafunzi 2,400 kwa wakati mmoja litakalokuwa na maabara nane
zenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 100 kila moja.
Prof.
Ndalichako anasema Serikali pia imekamilisha ujenzi wa jengo la utafiti
wa wanyama na wadudu kwa ufadhili wa mradi wa Eastern and Southern
Africa Centers of Excellence for Innovative Rodent Pest Management and
Biosensor Technology Development (ACE II, IRPM and BTD) na kuendelea na
ukarabati wa madarasa likiwemo jengo la Hay Building kwa lengo la
kuongeza nafasi za kufundishia na kujifunzia.
Mazao
ya Kilimo ni malighafi muhimu sana katika viwanda, hivyo ni utafiti ni
nguzo muhimu sana inayoweza kuleta kuleta ubunifu wa bidhaa, uboreshaji
wa bidhaa, kuongeza ufanisi wa huduma, tija na ubora wa utendaji katika
soko.
0 Comments