
Na WAMJW – Dar es Salaam
25/05/2020 Serikali imewataka
madereva wa malori nchini kuchukuwa tahadhari dhidi ya Virusi
vinavyosababisha ugonjwa wa Corona (COVID-19) hii ikiwa ni pamoja na
kuhakikisha wanakula vyakula ambavyo vitalinda kinga zao za mwili.
Rai hiyo imetolewa hivi karibuni
na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (WAMJW)
Ummy Mwalimu wakati akizungumza na baadhi ya madereva wa kampuni
mbalimbali za malori zinazosafirisha mizigo nje ya nchi waliofika
katika maabara ya Taifa ya afya ya jamii iliyoko mabibo jijini Dar es
Salam kwa ajili ya kupima kama wana maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa
Corona au la.
Waziri Ummy alisema ugonjwa wa
Corona bado upo ingawa maambukizi yamepungua jambo la muhimu ni kwa
wananchi kufuata maelekezo yanayotolewa na wataalamu wa afya hii ikiwa
ni pamoja na kuepuka mikusanyiko isiyokuwa ya lazima, kunawa mikono kwa
sabuni na maji safi yanayotiririka, kuvaa barakoa pia kukaa umbali wa
zaidi ya mita moja kati ya mtu na mtu.
“Nimefurahi sana kuwaona mko hapa
kwa ajili ya kupima virusi vya Corona kama mtakutwa hamna maambukizi ya
ugonjwa huu mjitahidi kula matunda yakiwemo machungwa, mananasi,
malimao, mboga za majani na tangawizi hii itawasaidia kinga zenu za
mwili kuwa juu. Pia muwapo safarini mnapopata nafasi msisahau kupiga
nyungu,’’, alisema waziri Ummy.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa maabara
ya Taifa ya afya ya jamii Ambele Mwafulango alisema pamoja na kupima
vipimo vya wagonjwa wengine kwa upande wa madereva walioko jijini Dar
es Salaam kwa siku wanawapima madereva 200 kwa madereva walioko mikoani
kuna utaratibu maalum wa kuchukuliwa sampuli ambazo zinatumwa Dar es
Salaam kwa ajili ya vipimo.
Majibu ya vipimo hivyo
yanatoka baada ya masaa 48 kama madereva hao watakutwa hawana
maambukzi watapewa vyeti ambavyo vinatumika kwa siku 14 hii itawasaidia
kwenda kupeleka mizigo nje ya nchi bila ya kupimwa tena katika nchi
wanazokwenda.
Mwafulango alisema kabla madereva
hao hawajafanyiwa vipimo vya Corona wanapimwa joto la mwili na wale
ambao watakutwa na joto la juu la mwili watapewa huduma ya haraka zaidi
ukilinganisha na wale ambao joto lao la mwili liko sawa.
“Madereva ambao tunawakuta hawana
maambukizi ya ugonjwa wa Corona tunawapa elimu ya kujikinga na ugonjwa
huu wanapokuwa safarini siku zote ’’.
“Katika maabara hii ya Mabibo tuna
mashine mpya tano ambazo ndani ya masaa 24 zinapima vipimo 1800 hii
imetufanya kupima vipimo vingi zaidi ukilinganisha na ilivyokuwa katika
maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii iliyoko ofisi za NIMR jijini Dar es
Salaam ambapo tulikuwa na mashine mbili ambazo zilikuwa zinapima vipimo
300 hadi 400 jambo ambalo lilikuwa linachelewesha utendaji wetu wa
kazi,’’, alisema Mwafulango.
Serikali imetenga utaratibu malum
kwa ajili ya madereva wa malori wanaosafirisha mizigo nje ya nchi ambao
wanafanyiwa vipimo vya ugonjwa wa Corona kabla ya kusafiri ili
kuhakikisha hawana maambukizi na kuwaepusha kupata usumbufu ambao
utajitokeza wanapokuwa safarini.
0 Comments