Serikali ya Afghanistan imewaachia huru wafungwa 900 ambao ni wanachama wa kundi la Taliban, ikiwa idadi kubwa zaidi ya walioachiwa tangu kusainiwa kwa makubaliano ya amani kati ya Marekani na Taliban.
Wafungwa hao wameachiwa mwishoni mwa kipindi cha siku tatu za
usitishwaji wa mapigano, kilichopendekezwa na Wataliban sambamba na
maadhimisho ya sikukuu ya Eid el-Fitr. Yapo matarajio kuwa kuachiwa kwa
wafungwa hao kutapunguza uhasama kati ya Wataliban na serikali ya mjini
Kabul, na afisa mmoja mwandamizi wa Taliban amelithibitishia shirika la
habari la Associated Press, kuwa kundi lake linatafakari kurefusha muda
wa usitishwaji wa mapigano.
Wafungwa wa Taliban waliachiwa kutoka gereza maarufu la Bagram, ambako bado kuna kambi kubwa ya jeshi la Marekani, na jingine la Pul-e-Charkhi mashariki mwa mji wa Kabul. Msemaji wa Taliban amesema kuwa wao pia wataachia idadi kubwa ya wafungwa wa kutoka upande wa serikali.
0 Comments