Baadhi ya waumini wa kanisa la KKKT dayosisi ya kusini kanisa kuu la mjini Njombe wakati wakiendelea na ibada ya pasaka.


Askofu mkuu wa KKKT dayosisi ya kusini DR George Fyavango akifafanua kuhusu jitihada zilizochukuliwa na kanisa hilo ili kuwanushuru waumini wake dhidi ya maambukizi ya virusi vya COVID-19

Moja ya kifaa cha kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona kilichowekwa nje ya kanisa la KKKT Njombe mjini

……....…..............................................

Na Amiri kilagalila,Njombe

Baadhi ya waumini wa kanisa la kiinjili la kirutheli Tanzania KKKT Dayosisi ya kusini wamesema utaratibu mpya wa uendeshaji wa ibada,harusi na misiba ulioanzishwa na kanisa hilo ili  kujikinga na maambikizi ya virusi vya Corona (COVID-19) umepunguza kiwango cha upendo na mshikano baina yao.

Kanisa la KKKT katika kujikinga na ugonjwa huo limepiga marufuku kupeana mikono pamoja na utamaduni wa kusalimiana kwa kugusana vifua huku pia likipunguza kiwango cha waumini kushiriki katika ibada hatua ambayo imewafanya kuongeza idadi ya ibada kutoka mbili hadi tatu kwa siku za jumapili.

Wakizungumza mara baada ya kuhitimisha ibada maalumu ya jumapili ya pasaka ambayo inawaunganisha waumini duniani kote kusherekea ufufuo wa yesu kristu kutoka kwa wafu baadhi ya waumini wa kanisa kuu la KKKT mkoa wa Njombe wanasema katika kipindi hiki cha pasaka hawana budi kujikabidhi kwa mwenyezi mungu ili aweze kuwanusuru na janga hilo tishio ulimwenguni huku tahadhali zaidi zikiendelea kuchukuliwa.

“Kwasababu hii hali tulikuwa hatujaizoea kwanza imetupunguzia upendo,tulikuwa ukikutana na mwenzio unakumbatiana hiyo kwa kweli inatuletea shida na utamaduni wetu ilikuwa ni kushikana mikono katika ibada na kusalimiana”alisema mmoja wa waumini wa kanisa hilo

Nae askofu mkuu wa KKKT dayosisi ya kusini DR George Fyavango akifafanua nje ya kanisa kuhusu jitihada zilizochukuliwa na kanisa hilo ili kuwanushuru waumini wake limepunguza muda wa ibada,kuongeza idadi ya Ibada ili kupunguza mrundikano huku mengine yakiwa ni kuzuia shughuli za harusi kwa muda na kutoa miongozo kwa waumini juu ya uendeshaji wa mikasa ya misiba katika jamii.

“Siku ya leo ni siku ya kufufuka kwake bwana wetu yesu kristo maana asingefufuka kusingekuwa na imani ya kikristu lakini kufufuka kwake na sisi tumepata ushindi,na kwenye kanisa letu tunaendelea na tunaendelea kusisitiza kwa sasa kuwa makini na kufuata taratibu za kiafya ili kuendelea kupambana na Corona”alisema askofu mkuu kkkt Dayosisi ya kusini Dr George Fyavangu