Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kwa mara ya pili, imetupilia mbali maombi ya aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu ya kujaribu kupinga uamuzi wa kuvuliwa ubunge.
Maombi
hayo yalitupwa mwishoni mwa wiki mbele ya Jaji Yose Joseph Mlyambina,
baada ya kukubaliana na pingamizi la awali lililowasilishwa na jopo la
mawakili kutoka ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali.
“Baada
ya kusikiliza hoja za mapingamizi na majibu, mahakama inakubaliana na
hoja za Serikali na inaona maombi hayana msingi kisheria kwa kuwa
sheria hairuhusu rufaa kwa kesi inayofafana na hiyo,”alisema.
Katika
maombi hayo namba 42 ya mwaka 2019 ya kutaka ridhaa ya Mahakama Kuu
kumruhusu kukata rufaa yaliyofunguliwa Oktoba 10, 2019,Tundu Lissu
alikusudia kupinga uamuzi wa yeye kuondolewa ubunge kwa mujibu wa Katiba
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Kanuni za Kudumu za Bunge
kutokana na kushindwa kuhudhuria vikao zaidi ya vitatu vya Bunge pasipo
ruhusa ya maandishi ya Spika.
Maombi
hayo yalipingwa vikali na mawakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Wakili
Mkuu wa Serikali kwa madai hayakustahili kusikilizwa kwa kuwa
yalikinzana na kifungu cha 5(2) cha Sheria ya Rufani kama
ilivyorekebishwa na Sheria ya Marekebisho ya Sheria Na. 25 ya mwana
2002.
Upande
wa Serikali, ulidai Lissu hakuwa na haki kisheria kupinga uamuzi wa
Jaji Sirilius Matupa ulitolewa Septemba 9, mwaka jana wa kumnyima ridhaa
kufungua shauri la mapitio ya kiutawala uamuzi ambao uliishia kwa yeye
kupoteza ubunge.
Ilielezwa
na mawakili wa Serikali, uamuzi wa Jaji Matupa haukupaswa kupingwa kwa
njia ya rufaa kwa kuwa uamuzi huo haukumaliza shauri kama inavyopaswa
kisheria.
Upande
wa Serikali uliishawishi mahakama katika kesi mbalimbali, Mahakama
iliamua kuwa rufaa haiwezi kukatwa kwa shauri ambalo limeisha katika
hatua za awali kama ilivyokuwa kwa kesi ya Lissu ambaye alikuwa akiomba
ridhaa ya kuwasilisha maombi ya mapitio na akanyimwa ridhaa kwa kuwa
maombi yake hayakuzingatia Sheria.
0 Comments