Na Zuena Msuya
Tabora
Waziri wa Nishati,
Dkt Medard Kalemani amewataka wakazi wa Mkoa wa Tabora kuongeza kasi ya kutumia
umeme unaopatikana mkoani humo kwakuwa matumizi yao yapo chini zaidi
kulinganisha na umeme unaozalishwa mkoani humo.
Dkt. Kalemani alisema
hayo wakati akikagua shughuli za usambazaji wa umeme vijijini katika Kijiji cha
Mizanza na kuwasha umeme katika Kijiji cha Busomeke wilayani Igunga mkoani
Tabora, Aprili 27, 2020.
Dkt. Kalemani alisema
kuwa mitambo ya kufua umeme iliyopo mkoani humo inauwezo wakuzalisha Megawati
42 za umeme ili itumike mkoa mzima lakini mpaka sasa matumizi ni Megawati 14
tu.
“Kwa nini ninyi
wakazi wa Tabora hamtaki kutumia umeme haliyakuwa tayari miundombinu imewafikia
na bei ya kuunganisha ni 27,000 tu! mitambo ya hapa Tabora inauwezo wa kufua
umeme wa Megawati 42, ninyi matumizi yenu hayafiki hata nusu ya umeme huo,hii
si sawa mtaharibu mitambo yetu kwakuwa mingine italazimika kuzimwa na ikizimwa
kwa muda mrefu itaharibika na nchi itapata hasara” alisema Dkt. Kalemani.
Aliwataka Viongozi wa
Serikali za Vijiji, Mitaa pamoja na Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) kuongeza
kasi ya kuhamasisha wananchi wa mkoa huo kuunganisha umeme katika nyumba zao.
Vilevile aliwataka
wananchi hao kuongeza shughuli za uzalishaji mali kama vile viwanda vidogo
vinavyotumia umeme ili kuongeza idadi ya matumizi ya umeme ambao mwingi hupotea
kwa kukosa watumiaji hali yakuwa bado wakazi wengi hawana huduma hiyo.
Katika ziara yake
hiyo, aliwasha umeme katika Kijiji cha Busomeke na kuwataka wananchi wa eneo
hilo kuendelea kulipia shilingi 27,000 ili waunganishiwe umeme.
Akiwa katika Kijiji
cha Mizanza, Dkt. Kalemani aliiagiza TANESCO, kuharakisha upelekaji wa nguzo
kijijini hapo, ili kuwapa fursa wakazi wa kijiji hicho kuunganishiwa umeme,
hivyo amewataka wakazi hao kulipia gharama za uunganishwaji na kutandaza
nyaya katika nyumba zao.
Aliendelea kusisitiza
kuwa miradi ya usambazi umeme vijiji hauna fidia, hivyo wananchi watoe
ushirikiano kwa wakandarasi na TANESCO pindi wanapopitisha miundombinu katika
maeneo yao kwa lengo la kurahisisha utekelezaji wa kazi hiyo.
Hata hivyo aliwataka
kutumia wakandarasi walioainishwa na TANESCO na wanaotambulika katika serikali
za mitaa na vijiji vyao ili kuepuka vishoka na watu wasiowaaminifu.
Sambasamba na hilo,
aliwaeleza kuwa wasikubali kulipia miundombinu ya umeme kama nguzo, nyaya,
mashineumba (Transfoma) wala mita za LUKU.
0 Comments