Baadhi ya wakulima wa parachichi pamoja mazao
mengine mkoani Njombe wakiwa katika mkutano wa wadau wa parachichi
uliokutanisha wakulima wa zao hilo,makampuni na watalaamu wa serikali ulioandaliwa
na asasi inayohudumia wakulima wa Parachichi na kilimo hai mkoani humo NSHDA na
kumsikiliza afisa kilimo wa halmashauri ya mji wa Njombe mara baada ya kueleza
changamoto zao.
Na Amiri Kilagalila,Njombe
Halmashauri ya mji wa Njombe imesema imekwisha baini mtandao mdogo wa wezi wa matunda ya parachichi mashambani nyakati za usiku wanaosababisha baadhi ya wakulima kuanza kukata tama dhidi ya kilimo hicho kilichopewa jina dhahabu ya kijani mkoani Njombe kutokana na thamani yake kwa sasa inayopelekea kukuza uchumi wa wakazi wa mkoa huo.
Afisa wa kilimo wa halmashauri ya mji wa Njombe Nolasco Kilumile kwa niaba ya mkurugenzi wa halmashauri hiyo,amebainisha hayo kwenye mkutano wa wadau wa parachichi uliokutanisha wakulima wa zao hilo,makampuni na watalaamu wa serikali ulioandaliwa na asasi inayohudumia wakulima wa Parachichi na kilimo hai mkoani humo NSHDA uliofanyika katika ukumbi wa Mlimani Motel kwa lengo la kujadili changamoto katika zao hilo na kuzifanyia kazi.
“Taarifa tulizo nazo tayari kuna kakikundi Fulani ka watu kanakotafuta hela kwa nguvu bila kufanya kazi shambani,tunafuatilia na tunaamini kwamba tutapata majibu lakini tunaomba wakulima tuendelee kushirikiana tukishirikiana na viongozi wa vijiji na mitaa lakini tunaamini msimu ujao haitajiludia,na tukimpata taratibu za kisheria zinafahamika ili iewe fundisho na kwa wengine”alisema Kilumile
Aidha ametoa rai kwa wanunuzi wa parachichi kupima matunda hayo nyakati za mchana na sio usiku ili kuondoa dhamira mbaya ya kuhitaji kumuibia mkulima nguvu yake katika vipimo kwa njia za kupima nyakati za usiku
“Utaratibu sikubaliani nao na nafikiri kwa kauli ya pamoja kwa kushirikiana na halmashauri pamoja na mkoa msimu ujao hatutegemei kuona mtu anapima parachichi usiku”alisema Kilumile
Awali katika mkutano huo wakulima wa matunda akiwemo Emilia Nyato,Domitila Njalika,Frolence Mwanyika wameieleza changamoto hiyo kuonekana kuwa kubwa kadri siku zinavyokwenda licha ya zao hilo kukubwa na changamoto zingine ikiwemo ulanguzi.
“Ni kero sana hili na haya makampuni yanahatarisha sana kilimo hiki yanpokuja kupima matunda usiku na hawa ndio wanaosababisha wizi kutokana na utaratibu mbovu tunaomba serikali iliangalie hili maana huko vijiji watu wanaumia sana”alisema Domitila Njalika
Licha ya changamoto hiyo wamesema hawatasahau mchango wa serikali ya awamu ya tano ya hayati Dkt John Pombe Magufuli katika kufungua masoko ya ndani na nje ya nchi ya malighafi hiyo.
Kuhusu uwekezaji wa mazao mengine mkurugenzi wa asasi inayohudumia wakulima wa Parachichi na kilimo hai mkoani humo NSHDA Ndugu Frenk Msigwa amesema NSHDA imepata soko la Choroko,Pilipili na Makademia maarufu karanga miti ambazo mahitaji yake ni makubwa katika nchi ya Ujerumani,Marekani,Denmark na Uholanzi na kwamba wakati umefika kwa wakulima kuchangamkia fursa hiyo.
0 Comments