Na Mwandishi wetu, Simanjiro
WALIMU wanawake wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, wametakiwa kujishughulisha na ujasiriamali ili kujiinua kimapato bila kuathiri muda wao wa kazi wa kufundisha wanafunzi.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Simanjiro, Zuwena Omary Jiri ameyasema hayo kwenye semina ya kuwajengea uwezo viongozi wa kitengo cha walimu wanawake wa chama cha walimu (CWT) cha wilaya hiyo.
Zuwena amesema endapo walimu hao wakijishuhulisha na ujasiriamali bila kuathiri kazi yao ya ufundishaji watajiongezea kipato na kujinyanyua kiuchumi.
Amesema uongozi wa wilaya ya Simanjiro unaitambua kazi ya ualimu na walimu kwa ujumla hivyo wanatambua mchango wao ni vizuri wakajiongezea kipato kwa njia hiyo.
“Nawasihi walimu wanawake kuwa wajasiri na kutokubali kushindwa, muwe wepesi kutatua changamoto zinazowakabili bila kukata tamaa,” amesema Zuwena.
Amesisitiza kuwa walimu wanawake wa eneo hilo ni wawajibikaji hivyo waendelee kufanya kazi ya kufundisha wanafunzi kwa bidii na kufuata sheria, taratibu na kanuni za kazi.
Mjumbe wa kitengo cha walimu wanawake Taifa na mwakilishi wa walimu wanawake mkoa wa Manyara, Tenisia Katukuru amehimiza upendo, ushirikiano na umoja ili kufanya kazi ya kwa urahisi.
Mwalimu Katukuru amewataka walimu wanawake kuwa walezi na washauri wazuri kwa watoto wa kike ili kuwaepusha na janga la walimu kujihusisha kimapenzi na wanafunzi.
Amewataka viongozi wa kitengo hicho wajitahidi kuwatembelea walimu wanawake na kubaini changamoto zinazowakabili na kuzitatua ili kutimiza wajibu wao ipasavyo.
Katibu wa CWT wilayani Simanjiro, mwalimu Nazama Tarimo alisema chama hicho kipo kwa ajili ya kutetea na kulinda haki na wajibu wa mwalimu.
Mwalimu Tarimo amewahimiza walimu kufanyia kazi kwa bidii na wawe wepesi wakukitumia na kukikimbilia chama hicho katika kutetea haki zao.
Mwenyekiti wa kitengo cha walimu wanawake wilayani Simanjiro, mwalimu Miriam Nyorona amewaomba wajumbe kuwa na umoja na mshikamano ili kitengo hicho kisongembele na kufanya kazi zenye tija kwa walimu.
0 Comments