Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa amesema kuwa kutoroka kwa Nabii wa Malawi na mke wake nchini humo ni jambo ambalo analifuatilia kwa karibu na ameahidi kuchukua hatua baada ya kupata taarifa za kina.
Nabii Shepherd Bushiri na mke wake Mary, wanakabiliwa na mashtaka ya ulaghai na utakatishaji wa fedha nchini Afrika Kusini.
Wawili hao walitoroka nchini Afrika Kusini wiki liyopita na kujisalimisha kwa polisi nchini Malawi baada ya Afrika Kusini kutoa kibali cha kukamatwa kwao.
Kupitia televisheni ya eneo, Rais Ramaphosa amesema tukio la wawili hao kutoroka "halikutakiwa kutokea".
"Bila shaka tutachukua hatua," Rais alijibu alipoulizwa ikiwa serikali inapanga kufanya lolote.
Baadhi ya taarifa zinasema kuwa muhubiri huyo aliyejitangaza mtume pamoja na mke wake walitoroshwa nchi humo kwa njia haramu na genge la watu ambalo linahusika na uuzaji wa magari yaliyoibwa nchini Afrika Kusini na kupelekwa Malawi.
Pia kuna baadhi ya vyombo vya habari Afrika Kusini vilivyosema kuwa nabii huyo alitoroka kwa kutumia ndege ya rais.
Hata hivyo serikali zote mbili zimekanusha madai hayo.
0 Comments