Na Omary Mngindo, Mapinga
MGOMBEA Ubunge Jimbo la Bagamoyo Mkoa wa Pwani Muharami Mkenge amewaondoa hofu wakazi wa Vijiji vinavyounda Kata ya Mapinga kuhusiana na kero ya mapori yasiyoendelezwa.
Aidha wananchi hao wametakiwa kukaa katika maeneo yao kwani kesi mahakamani zimekwisha, na kwamba atamfikishia kilio hicho mgombea Urais Dkt. John Magufuli, ili ayafutie umiliki wake kwani wananchi wa maeneo hayo wana mahitaji mengi yanayohusiana na ardhi.
Mkenge aliyasema hayo akiwa katika viwanja vya Mingoi Mpiji katani hapo, akiwa kwenye mkutano wa Kampeni akiambatana na viongozi wake akiwemo Meneja wa Kampeni Yahya Msonde, Katibu Gertrude Sinyinza, Hanipha Cheche wa UWT na wa Vijana Japhet Thibias ambapo alisema watapambana na suala hilo.
"Kuna taarifa kwamba mnaambiwa baadhi ya maeneo mnatakiwa kuondoka kwa madai kwamba ni ya watu, lakini hayo maeneo hayaendelezwi, pia kuna kesi ipo mahakamani, endeleeni kukaa hii kero nitaifikisha kwa Dkt. John Magufuli mtetezi wetu sisi wanyonge ili afute umilili wake," alisema Mkenge.
Kwa upande wake Msonde alisema kuwa Rais Dkt. Magufuli ameandika historia nyingine mpya ya wanafunzi zaidi ya milioni moja walioanza elimu ya msingi asipomalipo wanaoanza mitihani yao Oktoba 7 na 8, na kwamba wataofaulu watasoma sekondari bure.
"Wa-tanzania tunataka nini tena, Rais wetu Magufuli amefanya mengi katika kila sekta na wote tunayaona, kuanzia Oktoba 7 na 8 vijana wetu zaidi ya milioni moja wanafanya mithihani yao ya kumaliza elimu ya msingi, na wataofaulu wote watakwenda sekondari pasipo kulipia ada, tuichague CCM," alisema Msonde.
Nae mgombea udiwani Kata ya Mapinga Dismass Chandika alisema kuwa wakazi katani hapo wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya mto Mpiji, ambao kipindi cha mvua wakazi walibomolewa nyumba zao, huku akiishukiru serikali kwa jithihada za kuboresha miundombinu hiyo.
Kwa upande wake Meneja Kampeni wa mgombea wa udiwani Tabia Nassoro alimwambia Mkenge kuwa, mpango wa ujenzi wa Chuo Cha Ufundi VETA utakapokuwa tayari, wana-Mapinga tayari wana eneo lenye ukubwa wa eka 9 walilopatiwa na Chandika kwa ajili ya shughuli za maendeleo, hivyo kijengwe hapo.
0 Comments