Na Amiri Kilagalila,Njombe
Akiwasilisha taarifa ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa Serikali kwa Mwaka 2018/2019 mweka Hazina wa Halmashauri ya mji Njombe Bi. Dorcas Mkello amesema kuwa Halmashauri ilipata Hati inayoridhisha (Hati Safi) yenye masuala mawili ya msisitizo ambapo moja ni miradi ya maji kuhamia Ruwasa na pili ikiwa ni kesi za madai yenye kiasi cha Tshs. 215,384,844 ambapo kama uamuzi utatoka juu ya walalamikaji Halmashauri itatakiwa kulipa fedha hizo.
Wakitoa mapendekezo yao wakati wa kujadili hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali kwa hoja ambazo hazikufungwa baadhi ya Madiwani George Sanga na Sigrada Mligo wamesema kuwa msisitizo uliotolewa kwenye kesi za madai ni vyema Halmashauri ikaona uwezekano wa kufanya majadiliano na walalamikaji nje ya mahakama ili kuweza kupunguza gharama na usumbufu ambao halmashauri inaweza kuingia kwenye kuendesha kesi hizo.
Kuhusu suala la upungufu wa Watumishi 996 ikiwa ni miongoni mwa hoja zilizojadiliwa jambo linalozuia utendaji kazi za kila siku, Baraza limeshauri Halmashauri kuendelea kuomba na kufuatilia kibali cha kuajiri Watumishi wapya na kutenga bajeti ya mishahara yao licha ya kuwa halipo katika ngazi ya Halmashauri.
Hoja nyingine iliyojadiliwa ni Usimamizi wa Mapato yaliyokusanywa kupitia mashine za kukusanyia mapato (POS) yasiyopelekwa Benki ambapo kiasi cha Tshs. 24,562,752 ziliweza kubainika na Baraza limeshauri kuwa fedha za mapato zikiwa zinakusanywa ziwe zinawekwa benki au kwa wakala siku zilizokusanywa na ufuatiliaji wa mara kwa mara ufanyike kwenye mfumo ili wakusanyaji wasikae na fedha kwa muda mrefu.
Aidha kwa wale wote waliotumia fedha za makusanyo kinyume na utaratibu Halmashauri ihakikishe kuwa wahusika wote wanarejesha fedha hizo wanazodaiwa. Kwa upande wa Halmashauri kiasi cha Tsh. 17.345,050 zimeshapokelewa kushirikiana na polisi na Halmashauri imeanza kuzuia mishahara yao kuanzia mwezi uliopita kufidia madeni yao.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Njombe Bi. Ruth Msafiri ameipongeza Halmashauri kwa kazi kubwa iliyofanyika mpaka kupelekea hati safi na ameitaka Halmashauri kuhakikisha kuwa inazuia uwepo wa hoja za ukaguzi kwani nyingine hazina ulazima wa kuwepo.
“Kuna idadi kubwa ya hoja ambazo zinaepukika kama hoja za bima za pikipiki na magari. Kuhusu mikopo na marejesho ya vikundi naungana na serikali mikopo hii kutokuwa na riba. Ni vyema Idara ya Maendeleo ya Jamii iendelee kutoa elimu zaidi na ikaona utaratibu mzuri kuunda vikundi vyenye miradi mikubwa ya pamoja. Tuache kuona mikopo hii kama ni ya kisiasa bali ni kwa ajili ya kuwainua Wananchi wenye kipato cha chini.”Alisema Mkuu wa Wilaya
Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Njombe Bi. Katarina Tengia amelipongeza Baraza kwa usimamizi mzuri kwa kupata hata safi kwa miaka 4 mfululizo na ukusanyaji wa mapato uliovuka lengo.
“Mmefanikisha kwa kiasi kikubwa utekelezaji wa miradi mikubwa ikiwemo katika sekta ya Afya, Ujenzi wa Soko na Stendi Mpya ya kisasa bila kuwa na hoja. Naomba nitoe rai kwa Halmashauri kuhakikisha inaendelea kusimamia udhibiti wa mapato kulingana na uwezo mkubwa wa Halmashauri ulionao katika ukusanyaji mapato ili wakusanyaji wasiweze kuingia kwenye mitego na tamaa. Aidha Halmashauri iendelee kuhakikisha kuwa inajibu hoja zote kwa wakati na kusiwe na hoja za kujirudia katika kaguzi zijazo. Niwaombe kutumia kaguzi za ndani kama jicho la kutabiri kaguzi za mwisho.”Alisema Katibu Tawala
Katika mwaka 2018/2019 kulingana na ripoti Halmashauri ilikuwa na jumla ya hoja 42 kati ya hizo 15 ni hoja za nyuma na 27 hoja za mwaka husika.
0 Comments