TANGAZA NASI

header ads

Uzalishaji wa kahawa waongezeka wafikia tani 214,962

 

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma
 
WAZIRI wa Kilimo, Mhe Japhet Hasunga (Mb) amesema kuwa katika kipindi cha Serikali ya awamu ya Tano ya Dkt. John Magufuli zao la Kahawa limeweza kufikia uzalishaji wa tani 214,962 .
 
Ametoa kauli hiyo Jijini Dodoma wakati akizungumzia mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya Kahawa katika kipindi cha miaka minne ya serikali ya awamu ya tano na kusema kuwa kwa wastani kila mwaka imekuwa ikizalisha tani 51,777 ya kahawa nzuri ambapo uzalishaji huo uliwezesha taifa kuingiza fedha nyingi za ndani na za kigeni.
 
Amebainisha kuwa kwa upande wa wakulima katika kipindi cha miaka minne wameweza kujipatia jumla ya Trilioni 1.195 ambazo zimeenda kuwanufaisha wakulima wa zao hilo. 

“Lakini kama Taifa pia tumeweza kupata dola za marekani milioni 427.9 ambazo ni fedha za kigeni katika kipindi hiki kitu ambacho ni mafaniko makubwa kwa wizara,” Amesema
 
Alifafanua kuwa kwa wastani baada ya kuanza kwa zoezi la uandikishaji wa wakulima kwa lengo la kuweza kuwatambua ili kuwahudumia mpaka sasa wakulima 286,397wamesajiliwa.
 
Alisema hao ndio wakulima wadogo wadogo ambao wanajishughulisha na zao la kahawa katika mikoa 16 ambayo ameitaja na kueleza kuwa kuna wakulima wakuba ambao wana mashamba 101 ambao wanazalisha kwa kiwango kikubwa zao hilo.
 
Kuhusu suala la ajira ameeleza kuwa kwenye upande wa ajira zao hilo la kahawa limechangia ongezeko la ajira za watu kutoka millioni 2.3 hadi milioni 2.7 ambapo hao wote wamejiajiri au wameajiriwa na sekta hiyo na wanashiriki kwenye uzalishaji na mnyororo wa thamani.
 
Amefafanua kuwa mchango wa zao hilo katika uchumi wa Taifa kwenye upande wa sekta ya viwanda lina viwanda takribani 554 ambavyo vinajishughulisha katika uchakataji wa kahawa kutoka katika ngazi ya uzalishaji mpaka ulaji.
 
Waziri Hasunga amesema kuwa viwanda hivyo vipo katika madaraja tofauti hivyo kuchukua nafasi hiyo kumpongeza Rais na viongozi wengine wakuu kwa kazi kubwa waliyofanya katika kuhamasisha uzalishaji, kuongeza tija, na uzalishaji wa zao hilo.
 
Amesema katika jitihada hizo, wakati Serikali inaendelea na jitihada nyingine za kuongeza uzalishaji kilichofanyika ni kuamua kupunguza kodi mbalimbali ambazo zilikuwa zinapunguza mapato kwa mkulima.
 
“Tumefuta zaidi ya kodi na tozo 19 kwenye zao la Kahawa kwa hiyo sasa kodi hizo zimepungua na sasa hivi mkulima anaweza akanufaika zaidi na akapata fedha nzuri.
 
Sambamba na hilo, amesema kuwa uwekezaji umeongezeka katika utafiti ili kuweza kupata mbegu zilizo bora, zinazofaa kwenye kilimo cha zao hilo, zinazotumia maji kidogo, zenye kustahimili ukame na zenye kukinzana na magonjwa ya kila namna.
 
Waziri Hasunga ameeleza kuwa kuna aina nyingi za magonjwa yaliyokuwa yanalikabili zao hilo ambapo kwa sasa Taasisi ya utafiti cha Kahawa (TaCRI) kilichopo kwenye kanda nane kimefanya utafiti na kuja na mbegu 19 za kahawa aina ya Arabika ambayo ina onyesha mafanikio makubwa.
 
Amesisitiza kuwa pia kuna mbegu nyingine tano aina ya Robusta ambazo zote kwa pamoja ukizijumlisha zinapatikana aina 23 za mbegu zilizo bora zilizofanyiwa utafiti wa kina na kuweza kutumika.
 
Ameeleza kuwa baada ya uzalishaji huo kukamilika kazi kubwa ambayo serikali imefanya ni pamoja na kuongeza uzalishaji na ubora wa kahawa ndio maana inaendelea kusisitiza wakulima wakivuna kahawa wapeleke kwenye CPU ili kusimamia ubora ili ukiimarika zilete fedha nzuri.
 
Ameongeza kuwa sambamba na hayo kumekuwa na changamoto ya masoko lakini jitihada za serikali ya awamu ya tano zilizofanyika na maagizo ya viongozi wa juu wameifanya wizara kuanzisha utaratibu mpya wa namna ya kuuza kahawa.
 
Waziri Hasunga amebainisha kuwa awali kulikuwa na aina mbili za masoko ambazo ni soko la moja kwa moja ambapo wakulima kupitia vyama vyao vya ushirika wanaingia mkataba na wanunuzi wa nje ya nchi na kuuza moja kwa moja hivyo kujipatia fedha nzuri.
 
“Pia, kulikuwa na soko ambapo kahawa nyingine inauzwa katika minada ambapo utaratibu wa nyuma ni kuwa minada yote ilikuwa inafanyika mkoani Kilimanjaro kwenye bodi ya kahawa lakini toka mwaka jana tulifanya maamuzi kwamba vianzishwe vituo vya minada” Alikaririwa Waziri Hasunga na kuongeza kuwa
 
“Kama sote tunavyojua kwamba kahawa ni moja ya mazao ya kimkakati ambayo yanalimwa katika mikoa zaidi ya 16 hapa nchini ambayo ni pamoja na Songwe, Mbeya, Ruvuma, Kagera, Kilimanjaro, Arusha, Mara, Kigoma, Tanga, Morogoro, Njombe, Katavi, na Mwanza”
 
Zao la Kahawa linashika nafasi ya tatu katika kuchangia mapato ya Taifa ambapo zao la kwanza ni Korosho likifuatiwa na zao la Tumbaku.

Post a Comment

0 Comments